Jumamosi 28 Novemba 2026 - 07:44
Dhuluma Haidumu, Hata Serikali Haiwezi Kusimama Juu ya Dhuluma

Hawza/ Ayatullah Husseini Bushehri, katika hotuba ya Swala ya Ijumaa mjini Qum, ameuonya utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain kuhusu dhuluma zinazofanywa dhidi ya wanazuoni na vijana wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Akisisitiza kuwa utawala unaweza kudumu pamoja na ukafiri, lakini hauwezi kudumu pamoja na dhuluma, ametoa wito kwa viongozi wa Bahrain kuheshimu hadhi na heshima ya wanazuoni wa dini.

Akiendelea na hotuba yake, Ayatullah Husseini Bushehri alizungumzia jinai zinazofanywa na utawala wa Aal Khalifa, akisema: “Wanazuoni na vijana wa Bahrain wako gerezani, na sauti zao haisikiki popote. Hata hivyo, wanapaswa kufahamu kwamba wananchi wa Qum na wa maeneo yote ya nchi yetu wamesikia sauti ya dhuluma wanayofanyiwa, na wanawaombea ili waachiliwe huru. Tunawaomba viongozi na serikali ya Bahrain kuhifadhi heshima ya wanazuoni wa dini.”

Imam wa Swala ya Ijumaa ya Qum aliendelea kusema: “Katika riwaya imekuja kwamba:

«الْمُلْكُ يَبْقَى مَعَ الْكُفْرِ وَلَا يَبْقَى مَعَ الظُّلْمِ»

‘Utawala unaweza kudumu pamoja na ukafiri, lakini hauwezi kudumu pamoja na dhuluma.’

Viongozi wa Bahrain wanapaswa kujifunza kutokana na historia ya namna Shah wa Iran alivyowashughulikia wanazuoni na wananchi, ambapo alikuwa akiwafukuza uhamishoni na kuwafunga gerezani. Matokeo ya vitendo hivyo yalikuwa ni kutokea Mapinduzi ya Kiislamu.”

Nafasi ya Bibi Fatimah Zahraa (sa) na Heshima ya Mwanamke katika Uislamu

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Husseini Bushehri aliwapongeza Waislamu kwa mnasaba wa kuzaliwa Bibi Fatimah Zahraa (sa) na Siku ya Mwanamke, akisema: “Bibi Fatimah Zahraa (sa) alikuwa Ummu Abiha (mama wa baba yake). Ingawa alikuwa na nafasi ya kuwa mtoto wa baba yake, lakini alikuwa akimhudumia baba yake kama mama anavyomhudumia mtoto wake.”

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza za Kielimu za Qum alieleza kuwa; maadui zetu wanatuhusisha na madai kwamba mwanamke katika Uislamu hana nafasi ya kushiriki katika shughuli za kijamii. Hata hivyo, uwepo wa Bibi Fatimah Zahraa (sa) katika vita vya Uhud na kuwahudumia majeruhi, pamoja na hotuba yake ya Fadakiyyah, ni ushahidi unaoonesha nafasi na ushiriki wa mwanamke katika jamii kwa mujibu wa Uislamu.

Akinukuu riwaya isemayo:

«كَانَ إِذَا دَخَلَ عَلَيْهَا قَامَتْ إِلَيْهِ وَرَحَّبَتْ»

Alieleza kuwa; katika riwaya hiyo imeelezwa kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww), Bibi Fatimah (sa) alipoingia mbele yake, hakuwa akisimama tu kwa ajili yake, bali pia alikuwa akienda kumpokea. Jambo hili linaonesha utukufu na nafasi kubwa ya Bibi Fatimah Zahraa (sa).

Imam wa Swala ya Ijumaa ya Qum aliendelea kusema: “Siku moja, mwanamume mmoja alimtuma mke wake kwa Bibi Fatimah Zahraa (sa), ili akamuulize iwapo wao ni miongoni mwa Mashia au la.

Bibi Fatimah Zahraa (sa) akamjibu: ‘Ikiwa utatekeleza yale tunayokuamrisheni na kujiepusha na yale tunayokukatazeni na kukuhadharisheni nayo, basi utakuwa miongoni mwa Mashia wetu. Vinginevyo, kamwe hutakuwa miongoni mwa Shia wetu.’”

Moyo Unapokosa Uchamungu, Hujazwa na Fitna za Dunia

Katika hotuba yake ya kwanza, Ayatullah Husseini Bushehri alisema kuwa Imam Ali (as) amesema:

«خُلُوُّ الْقَلْبِ مِنَ التَّقْوَى يَمْلَؤُهُ مِنْ فِتَنِ الدُّنْيَا»

“Moyo wa mwanadamu hauwezi kubaki mtupu. Kwa hiyo, moyo unapokosa uchamungu, hujazwa na fitna na majaribu ya dunia.”

Akizungumzia mwenendo wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) katika kukabiliana na maadui, alisema kuwa: Mitume wa Mwenyezi Mungu, akiwemo Mtume Muhammad (saww), walikuwa na malengo maalumu katika kukabiliana na maadui zao ambayo yalikuwa yamejengwa juu ya misingi na kanuni mbalimbali.

Imam wa Swala ya Ijumaa ya Qum aliendelea kueleza kuwa; kuondoa shirki na kusimamisha uadilifu na usawa ni miongoni mwa misingi ya namna Mtume (saww) alivyoshirikiana na kukabiliana na maadui zake.

Alisema kuwa uadilifu ni jambo ambalo wanadamu wamelikosa na kulihitaji sana. Wanadamu wote wanapenda uadilifu, hata kama wao wenyewe si waadilifu.

Uadilifu ni Nguzo Muhimu katika Maisha ya Mwanadamu

Ayatullah Husseini Bushehri aliuelezea uadilifu kuwa ni suala muhimu na la msingi katika maisha ya mwanadamu, akiongeza kuwa umuhimu wake ni mkubwa kiasi kwamba baadhi ya watu hujitolea mali zao, maisha yao na heshima zao ili kusimamisha uadilifu katika jamii. Wengine hutumia kalamu zao na ndimi zao zenye uwezo wa kueleza ukweli ili kuhakikisha kwamba uadilifu unatawala katika jamii ya Kiislamu.

Aidha, alieleza kuwa katika historia kumekuwepo watu ambao hata kama hawakuwa Waislamu, majina yao yameandikwa katika historia kwa uadilifu na wema kutokana na juhudi zao za kusimamisha uadilifu ndani ya jamii.

Imam wa Swala ya Ijumaa ya Qum alisema kuwa uadilifu ndio utakaohitimisha hali ya ulimwengu huu. Wanadamu wote duniani, hususan Mashia, wanangojea kudhihiri Mwokozi ili uadilifu utekelezwe. Daima tunarudia kauli isemayo:

«يَمْلَأُ اللهُ بِهِ الْأَرْضَ قِسْطاً وَعَدْلًا كَمَا مُلِئَتْ ظُلْماً وَجَوْراً»

“Mwenyezi Mungu kupitia kwake ataijaza ardhi uadilifu na usawa, kama ambavyo hapo awali ilikuwa imejazwa dhuluma na uonevu.”

Akirejelea Aya ya 25 ya Suratul-Hadid, inayosema:

«لَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا بِالْبَيِّنَاتِ وَأَنْزَلْنَا مَعَهُمُ الْكِتَابَ وَالْمِيزَانَ لِيَقُومَ النَّاسُ بِالْقِسْطِ»

“Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu kwa hoja zilizo wazi, na tukateremsha pamoja nao Kitabu na Mizani, ili watu wasimamishe uadilifu.”

Alisema kuwa: Mwenyezi Mungu katika Aya hii anaeleza kwamba aliwatuma Mitume kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu ili wapate uelewa na mwamko, na wao wenyewe waweze kusimamisha uadilifu katika jamii.

Alifafanua kuwa katika Aya hii haijasemwa kwamba Mitume ndio wanaosimamisha uadilifu, bali utekelezaji wa uadilifu unapaswa kufanywa na wananchi wenyewe.

Uadilifu Unaweza Kuwa Sababu ya Watu Kuupenda Uislamu

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza za Kielimu za Qum, akisisitiza umuhimu wa uadilifu alikumbusha kwamba; maadui wa Uislamu wanapoona watu wenye dhamana na majukumu ya uongozi wakitenda uadilifu, hata wao huanza kuvutiwa na dini yetu, kwa sababu kila mtu anautafuta uadilifu.

Kwa sababu hiyo, alisema kuwa; uadilifu ulikuwa miongoni mwa misingi muhimu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saww) katika kukabiliana na maadui zake. Imam wa Swala ya Ijumaa ya Qum alisisitiza kuwa jamii ya kidini inapouona uadilifu, imani yake katika dini huimarika zaidi. Vilevile, jamii isiyo ya kidini inapouona uadilifu, huanza kuvutiwa na dini.

Athari za Shahada ya Kiongozi Shahidi katika Kuamsha Jamii

Ayatullah Husseini Bushehri alisema kuwa: Imam Khomeini (ra) na Kiongozi Shahidi walikuwa wakitoa wito kwa wananchi kushiriki katika jihadi na shahada wakati wa Vita vya Ulinzi Mtakatifu vya miaka minane na vita vya siku 12, na wananchi walikuwa wakiitikia wito huo.

Hata hivyo, alisema kuwa; kuuawa kishahidi Kiongozi Shahidi akiwa pamoja na familia yake kulisababisha mabadiliko makubwa katika jamii na kuibuka kwa jamii iliyopata mwamko na kusimama upya kwa ajili ya kutekeleza wajibu wake.

Alifafanua kuwa, hali hiyo ilitokana na wananchi kuona kwamba kiongozi wa jamii alikuwa akiamini kwa dhati yale aliyokuwa akiyasema, na kwamba yeye mwenyewe alikuwepo katika medani ya jihadi na shahada. Jambo hilo liliwafanya wananchi kuyaweka pembeni matatizo na tofauti zao, na kujitokeza kwa wingi katika medani.

Katika kuhitimisha hotuba yake, Imam wa Swala ya Ijumaa ya Qum alinukuu kauli ya Imam Ali (as), akisema:

«الْعَدْلُ أَسَاسٌ بِهِ قِوَامُ الْعَالَمِ»

“Uadilifu ni msingi ambao ulimwengu umesimama juu yake.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha